(Nairobi) - Mamlaka za Tanzania zimewakamata kimakosa wanaodaiwa kuwa waandaji wa maandamano na wafuasi wa upinzani kabla ya maandamano ya nchi nzima yaliyoitishwa Desemba 9, 2025, Human Rights Watch ilisema leo. Serikali ikomeshe ukandamizaji wake na kuwaachilia mara moja wale wote waliozuiliwa kiholela.
Wanaharakati wamewataka watu kuandamana kwa amani katika Siku ya Uhuru wa Tanzania, inayojulikana kama D9, kupinga polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Serikali ilifutilia mbali sherehe za Uhuru baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza fedha za sherehe hizo zitumike kurejesha miundombinu iliyoharibika wakati wa machafuko ya uchaguzi. Mnamo Desemba 3, polisi walitangaza kuwa walikuwa wakiwakamata watu wanaofanya "makosa ya mtandaoni" na wamekuwa "wakifuatilia kwa karibu" wito wa maandamano kupitia mitandao ya kijamii
"Serikali ya Tanzania inafanya muendelezo wa hali ya tahadhari na hofu iliyokuwepo kabla ya uchaguzi kuzuia maandamano zaidi," alisema Oryem Nyeko, mtafiti mkuu wa Afrika kutoka Human Rights Watch. "Mamlaka zinapaswa kukomesha ukandamizaji wao na kuheshimu haki ya Watanzania ya kutoa maoni yao kwa amani."
Tangu katikati ya Novemba, polisi wamethibitisha kukamatwa kwa wanaharakati 10 na wafuasi wa upinzani wa kisiasa kwa machapisho ya mtandaoni yanayohusiana na maandamano yaliyopangwa. Katika visa kadhaa, polisi walithibitisha kukamatwa kwa watu hao siku chache baada ya mitandao ya kijamii kuanza kusambaa kuwa watu wasiojulikana wakiwa wamevalia kiraia wamewateka nyara washukiwa hao.
Mnamo Novemba 13, polisi walitangaza kuwa wamemkamata Ambrose Leonce Dede katikati mwa Tanzania wilaya ya Ikungi. Walimshutumu kwa "kupanga na kuendeleza uhalifu kupitia Kikundi cha WhatsApp ... chini ya mwavuli wa maandamano ya amani." Jeshi la Polisi lilimtaja Dede kuwa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama kikuu cha upinzani, na kuwaonya wananchi kujiepusha na kujihusisha na vikundi vya mawasiliano mtandaoni vinavyoendeshwa na watu waliojipanga na wanaoendelea kujipanga kufanya uhalifu nchini kwa kisingizio cha maandamano ya amani.
Mnamo Novemba 19, polisi mkoani Geita walithibitisha kuwa wanamshikilia Kibaba Furaha Michael, mfanyakazi wa hospitali na msimamizi wa kikundi cha WhatsApp cha madaktari Tanzania, siku mbili baada ya kuripotiwa kutoweka. Mtu anayefahamu kesi hiyo aliiambia Human Rights Watch kwamba kukamatwa huko kulionekana kuhusishwa na machapisho ambayo Michael alitoa katika kundi hilo akihimiza ushiriki katika maandamano yajayo.
Novemba 21, polisi jijini Mbeya walimkamata mwalimu Clemence Mwandambo anayefahamika kwa kuikosoa serikali mtandaoni na kumtuhumu kwa kusambaza ujumbe wa “uchochezi” kwenye Facebook na Instagram.
Mnamo Novemba 28, polisi walithibitisha kuwa wanamshikilia Winfrida Charles Malembeka kwa madai kwamba alikuwa amechapisha "taarifa za uchochezi" na "alichochea vurugu na maandamano" Desemba 9 kupitia mitandao ya kijamii. Polisi hawakubainisha maudhui au majukwaa.
Mamlaka imeongeza ukamataji wa wafuasi wa Chadema kabla ya maandamano bila ya msingi wa kisheria
Novemba 21, polisi walitangaza kuwa wanamshikilia Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kyela, Victoria Swebe pamoja na wenzake watatu kwa tuhuma za uchochezi. Swebe alikuwa ameripotiwa kutoweka siku tatu zilizopita. Chadema iliripoti kuwa mwanachama mwingine wa chama hicho, Shabani Mabala, alitekwa Novemba 29 na watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi. Siku hiyo hiyo, Chadema iliripoti kuwa polisi walimkamata mfuasi mwingine wa chama hicho, Lucy Shayo, mkoani Tanga na kumshikilia bila kufunguliwa mashtaka.
Kabla ya maandamano ya Desemba 9, mamlaka inaonekana kuzidisha unyanyasaji wa kidijitali na ufuatiliaji wa wanaharakati, Human Rights Watch ilisema.
Mnamo Novemba 12 majira ya saa 3 usiku, polisi walivamia hoteli moja jijini Dar es Salaam na kuchukua kompyuta mpakato, simu na vitambulisho vya wafanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu walipokuwa wakifanya kazi hotelini hapo. Maofisa hao waliwaambia watumishi hao wafike katika Ofisi ya Makosa ya Jinai Kanda ya Dar es Salaam asubuhi iliyofuata, ambako vitu vyao vilirejeshwa. Wakili anayefahamu kesi hiyo alisema kuwa polisi waliwahoji wafanyakazi hao kuhusu madai ya kufanya utafiti kuhusu ghasia za uchaguzi.
Kampuni ya kiteknolojia ya Meta iliripoti katika ripoti yake ya Desemba ya Vikwazo vya Maudhui kwamba imeondoa na kuzuia upatikanaji wa maudhui nchini Tanzania kufuatia ombi la Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania la kutaka kuzuia ufikiaji wa akaunti tatu za Instagram kwa madai ya kukiuka sheria za Tanzania. Meta ilisema vipengele hivyo ni pamoja na "wito wa maandamano ya amani na yana ukosoaji wa serikali wakati wa kipindi cha uchaguzi."
Tarehe 28 Novemba, ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam ulitoa taarifa ikiwaonya raia wa Marekani kwamba "vikosi vya usalama vimepekua vifaa vya kielektroniki ili kupata ushahidi wa uhusiano na machafuko au maudhui nyeti ya kisiasa."
Mashirika kadhaa ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Human Rights Watch, wameibua wasiwasi kuhusu mauaji ya kiholela, kutoweka kwa nguvu, na kuwekwa kizuizini kiholela kwa waandamanaji, viongozi wa upinzani na wanaharakati wa mashirika ya kiraia kufuatia uchaguzi.
Mnamo Novemba 18, Ofisi ya Rais ilitangaza kuundwa kwa tume huru, inayojumuisha viongozi wa zamani wa serikali na watumishi wa umma waliostaafu "kuchunguza matukio yaliyosababisha uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu." Tume haina wanachama wa vyama vya kiraia au upinzani wa kisiasa. Mnamo Novemba 29, Rais Hassan aliitaka tume hiyo kuchunguza ni nani aliyelipa "vijana hao walioingia barabarani kudai haki."
Serikali inapaswa kuangalia upya mamlaka ya tume, kuchukua hatua za kuhakikisha uwajibikaji bila upendeleo kwa tuhuma za mauaji yanayohusiana na uchaguzi, kupigwa na kushambuliwa na vikosi vya usalama na watu wasiojulikana, kuhakikisha ushiriki mpana katika uchunguzi, na kuwawajibisha waliohusika, Human Rights Watch ilisema.
Sheria za Tanzania na za kimataifa zinahakikisha uhuru dhidi ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela na kulinda haki ya kila mtu ya kutoa maoni kwa uhuru, kushirikiana na kukusanyika kwa amani bila vikwazo vyovyote visivyofaa. Mashirika ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, wanapaswa kuzihimiza mamlaka za Tanzania kuzingatia wajibu huu, kukomesha unyanyasaji wa wakosoaji, na kushirikiana kufanya uchunguzi huru, unaozingatia haki kuhusu unyanyasaji uliotokea baada ya uchaguzi.
"Ni muhimu sana kwa wakati huu muhimu kwa mamlaka za Tanzania kuzingatia katika kuhakikisha haki na uwajibikaji kwa ukiukaji mkubwa wa haki baada ya uchaguzi," Nyeko alisema. "Jambo lolote pungufu ya hili litakuwa ni dharau kwa waathirika wengi na kwa haki za kimsingi za Watanzania."